Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amelalamikia uamuzi wa Bunge unaopendekeza yeye na baadhi ya vigogo wachukuliwe hatua, akidai kuwa haukuwa wa haki kwa wote waliotuhumiwa na ulifanywa kwa hasira na kufuata mkumbo.
Bunge liliazimia Jaji Werema kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria kutokana na kuipotosha Serikali kuhusu malipo ya Sh306 bilioni kutoka akaunti ya Tegeta Escrow, akishauri fedha hizo zilipwe kwa Kampuni ya IPTL iliyo na mkataba wa ufuaji umeme na Tanesco bila ya kukata kodi.
Jaji huyo hakusalimu amri wakati Bunge likijadili tuhuma dhidi yake, akisema anaamini alichofanya na kutaka abebeshwe msalaba na wakati fulani alishiriki kupendekeza jinsi ya kufikia maazimio ya Bunge dhidi ya watuhumiwa.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu maazimio ya Bunge katika sakata la uchotaji wa fedha hizo, jaji Werema alisema:
“Kilichofanywa na Bunge ni mob justice (uamuzi wa kufuata mkumbo) kwa sababu hata waliowatuhumu, hawakupewa nafasi ya kujieleza. (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna) Tibaijuka na (mmiliki wa hisa za IPTL, James) Rugemalira hawakusikilizwa lakini wamehukumiwa… ilionekana dhahiri jinsi Bunge linavyoingilia uhuru wa Mahakama kwa kutoizingatia hukumu ya Jaji (John) Utamwa,” alisema Jaji Werema.
“There was no justice at all (hakukuwa na haki kabisa). Bado haijathibitika ukweli kuhusu fedha zile kama ni za umma au la. Ninyi waandishi bado mna nafasi ya kufanya uchunguzi ili muwaeleze wananchi ukweli kuhusu wasichokijua,” alisema Werema ambaye mara nyingi hukataa kuzungumza na waandishi wa habari siku za Jumapili kwa madai ya kupumzika.
Werema alitaka pia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iueleze umma ili kuondoa sintofahamu iliyopo juu ya mmiliki halali wa fedha zilizokuwamo katika akaunti hiyo.
Kauli ya Jaji Werema inafanana na iliyotolewa na Waziri Tibaijuka kupitia gazeti hili jana akisema anasikitika kwa kuwa hakupewa nafasi ya kujitetea dhidi ya tuhuma za kunufaika na fedha hizo.
Tibaijuka pia alisema anashangaa jinsi gani jina lake liliingizwa kwenye ripoti ya Kamati ya PAC, wakati halikuwapo katika ripoti ya CAG.
Juzi Bunge lilihitimisha mjadala wa kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow, kwa kupitisha maazimio manane, ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Bunge hilo pia liliwawajibisha wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme (Tanesco) na liliwavua nyadhifa zao wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za Bunge ambao ni mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja na Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge.
Akisoma maazimio hayo juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema kuwa baadhi ya watu waliochukua fedha hizo ni viongozi wa umma na maofisa wa Serikali kama mawaziri, majaji, wabunge, wenyeviti wa kamati za Bunge, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi.
Maazimio yaliyopendekezwa ni pamoja na kulitaka Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi ili kukabiliana na kile kinachoonekana kuwa ni rushwa katika utoaji wa mabilioni yaliyokuwemo katika akaunti hiyo.
Azimio la tatu lilikuwa ni kuzitaka Kamati za kudumu za kuwavua nyazifa zao za wenyeviti wa kamati husika za Bunge kabla ya mkutano wa 18 wa Bunge hilo na la nne likiwa ni kumwomba Rais aunde tume ya kijaji kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Pia kulikuwa na azimio la kuzitaka mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Benki ya Stanbic na benki nyingine yoyote itakayogundulika kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow, kuwa taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu. Zitto aliiomba Serikali iandae na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyounda Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa lengo la kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulikia mapambano na udhibiti wa vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi.
Katika azimio la saba na nane, Zitto aliitaka Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco na Serikali kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme mapema iwezekanavyo kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge la Bajeti ya Serikali.
Chanzo: Mwananchi, 1 Disemba 2014